Friday, 21 June 2013

Mambo Yanayosabisha Biashara Ishindwe Kustawi



Kuna sababu nyingi zinazosababisha biashara kushindwa kuendelea na hatimaye kufa. Sababu tatu kuu zinazokwamisha biashara kuendelea, kwanza ni sababu binafsi za mjasiriamali, sababu za kibiashara, na sababu za mazingira.

1.Sababu binafsi za mjasiriamali. Tafiti nyingi zimebainisha kwamba mjasiriamali anachangia kufanikiwa kwa biashara au kushindwa. Umri, uzoefu, aina ya biashara  unayoifanya, historia ya familia, na kiwango cha elimu pia inachangia biashara kufanya vizuri au kushindwa kushamiri. Pia ukosefu wa ari ya mafanikio na kutojituma kufanya kazi kwa bidii ni sababu nyingine. Tafiti pia zinaonyesha kuwa mjasiriamali yeyote ambaye hajawahi kuwa kiongozi popote pale ana uwezekano mkubwa wa kushindwa kusimamia biashara ukilinganisha na mtu ambaye amewahi kuwa kiongozi shuleni au katika vikundi mbalimbali kwa mfano, jumuiya za kidini.

Kwa upande mwingine, tafiti zinaonyesha kwamba biashara zinazoanzishwa na kuendeshwa na mtu mmoja zina nafasi kubwa ya kutofanikiwa ukilinganisha na biashara zinazoendeshwa na mtu zaidi ya mmoja.

Ushauri, ili uweze kufanikiwa katika biashara kubali kushika nafasi za uongozi sehemu yoyote iwe kwa mwanafunzi shuleni au chuoni, iwe katika jamii na jumuiya za dini, kwani inaaminika kwamba ukiweza kuongoza watu ni rahisi kuendesha na kuitawala biashara yako.

Pia ubunifu na kujenga ari ya kujituma husaidia biashara kukua, kama umeweka msimamizi wa biashara hakikisha kila siku unapata taarifa muhimu juu ya mwenendo wa biashara hata kwa njia ya ujumbe mfupi wa meseji.

2.Sababu za kibiashara. Sababu za kibiashara zinajumuisha ubora wa bidhaa au huduma, wateja na soko kwa ujumla. Tafiti pia zinabainisha kuwa anayefanya biashara bila kufuata kanuni za kimasoko mfano huduma kwa wateja, bei, sehemu ya biashara, ana nafasi kubwa ya kushindwa katika biashara.

Pia biashara zinazoanzishwa kwa mtaji mdogo kulinganisha na mahitaji halisi hua zinakosa takwimu sahihi za biashara na hazina kumbukumbu za mahesabu na mwisho wa siku zinakosa mtaji kidogo uliokuwapo. Biashara zinazoendeshwa bila kupata ushauri wa kitalaam zina uwezekano mkubwa wa kufa mapema.

3.Sababu za mazingira. Sababu za mazingira zinahusisha biashara za kuiga, ushindani mkali katika soko na kupanda haraka kwa gharama za uzalishaji.

Mjasiriamali kushindwa kuendesha biashara ni fursa ya kufanikiwa kwa biashara nyingine kutokana na ukweli kwamba mjasiriamali hujifunza kutokana na makosa mbalimbali.

Kama  atarekebisha makosa na kuanza upya biashara ya awali au kubadilisha biashara kuna uwezekano mkubwa wa kufanikiwa.

Endapo mjasiriamali anashindwa kuendesha  biashara, inatoa ishara kuwa kuna kitu hakiko sawa hivyo marekebisho anapaswa kufanya marekebisho na  kuangalia upya vihatarishi vya biashara na kuamua namna ya kufanya ili kuvipunguza. Jenga urafiki na watalaamu mbalimbali ufaidi ushauri wao kuboresha biashara yako.